Monday, January 3, 2011

JAMANI MUOKOE MWENZI WAKO IKIWA ANATOA HARUFU MBYA BY KHADIL

Jambo la kwanza unapoanza kusoma safu hii ni kumshukuru Mungu kwa kukuwezesha kufika leo, ikiwa ni siku ya tatu ya mwaka mpya wa 2011. Wema wake ni mkubwa mno kwako ndiyo maana amekubakiza, kwa hiyo ni deni kwako kuulipa.

Ilikuwa mbaya kwa wale waliopata misukosuko ya hapa na pale. Inauma kumpoteza yule uliyempenda iwe kwa ugomvi, kifo au sababu yoyote ile. Natumia fursa hii kutoa pole kwa kila aliyefikwa na baya lolote mwaka 2010.

Turudi kwenye mada yetu, leo ikiwa ni sehemu ya nne. Wiki iliyopita niliandika namna yas kushughulikia nywele za kwapa pamoja na zile nyeti. Bila shaka utakuwa umepata kitu cha kuzingatia katika kuboresha uhusiano wako.

HARUFU
Msomaji utakuwa shahidi kuhusu hili kwamba tatizo la harufu ya mwili hasa maeneo nyeti, ni kitu ambacho kinawaaibisha wengi. Wake kwa waume wanaumbuliwa na hili. Kama hujaona, basi umesikia au kusimuliwa.

Watu wengi hawana simile, wasipowaeleza wenzi wao kuhusu kero ya harufu, basi watakwenda kuyazungumza mitaani kwa marafiki. Wote hao wana kasoro ya kutojua maana ya mapenzi na wajibu wao.

Rafiki yangu mmoja aliwahi kunisimulia namna alivyomfukuza mpenzi wake wa ‘kula na kuondoka’ chumbani gesti baada ya kumbaini anatoa harufu mbaya, hasa sehemu nyeti. Alisukumwa zaidi na ujana.

Aliniambia: “Justina ni mzuri tu kwa juu, nimeingia naye chumbani duh! Nilishindwa kuvumilia harufu, nikamtimua chumbani.” Ni uamuzi wake lakini iliniuma mno.

Niliwaza sana kuhusu namna yule dada alivyoumia. Ni mrembo lakini alitendwa na kijana ambaye alikosa uungwana. Si kila ukweli unafaa. Unatakiwa uwe sahihi mdomoni lakini siyo kung’ang’aniza ukweli wako.

Hapa namaanisha kuwa unaweza kusema ukweli lakini ukakosa uungwana. Mfano hai ni huyo rafiki yangu. Inawezekana ni kweli huyo mpenzi wake anatoa harufu iliyomkera ila alipungukiwa busara katika kumfikishia ujumbe.

Stori nyingine ni tukio ambalo nililishuhudia kwa macho yangu. Siku moja nilikwenda kumtembelea rafiki yangu lakini kilichotokea ni kama ule msemo wa “ukitembea uchi ndiyo unakutana na mkwe barabarani.”

Huyo rafiki yangu akavua viatu, mkewe bila hata kunionea aibu mimi mgeni, akamrudi mumewe. Akamwambia: “Aah … (alitaja jina la rafiki yangu), miguu yako inanuka bwana, hizo soksi hufui? Unatuchafulia hali ya hewa.”

Kauli hiyo ilimnyong’onyeza rafiki yangu, akawa mpole. Aliniangalia kwa jicho lenye kusema: “Naomba uyavumilie ya nyumba hii.” Kimsingi mke wa ndugu yangu hajastaarabika hata kidogo.

Sikupata picha ni nini alichofundishwa kwenye ‘kitchen party’. Mwanamke mstaarabu hawezi  kuwa mropokaji kwa kiwango hicho. Alichosema ni kweli lakini alivyofikisha ujumbe haikuwa sahihi.

UNAWEZA KUEPUKA FEDHEHA!
Muhimu ni wewe kujitunza kwanza kabla hujaumbuliwa. Jifanyie usafi na uhakikishe unakuwa mfano bora kwa wengine. Iwe ni mwanamke au mwanaume unaweza, kimsingi ni dhamira yako ndiyo inayokutuma.

Hata kama nafundisha mwenzi wako asikuchakachue unapotoa harufu mbaya, kilicho bora ni wewe kuheshimu utu wako kwa kujiweka nadhifu. Mwenzio anapokukuta msafi, unajiongezea alama za kupendwa. 

MWENZI ANANUKA, DAWA NI HII
Usithubutu kumuanika mwenzi wako kwa ubaya. Jaribu kumueleza yeye kwa nafasi yake mkiwa wawili, tena kwa lugha laini ili aweze kukuelewa. Penda kufundisha badala ya kutoa matamshi ya kuudhi.

Fundisha kwa kuonesha mfano, kama soksi zake zinatoa harufu, hupaswi kumnanga mbele za wageni. Shughulikia kwa namna bora kabisa. Wewe ni mwanamke, mfulie kwani usipofanya hivyo mwisho ni aibu yenu wote.

Kwa kawaida wewe unapochekesha, jamii humtazama zaidi mwenzi wako. Mathalani unavaa nguo chafu au umezunguka mtaani uchi, aibu itakuwa kwa mwandani wako kwa maana kila mtu atamsema kwako. Mke wa fulani au mume wa fulani.

Mkeo mvivu anashindwa kufanya usafi, nawe upo ‘bize’, kilichopo mbele yako ni kuajiri mfanyakazi ili akuepushie aibu. Ashughulikie usafi wa kuonekana ili wewe uanze kudili na ule wa faragha.

HARUFU YA FARAGHA
Umehakikisha kila kitu kipo kwenye mstari lakini bado mwenzi wako anatoa harufu inayokera hasa eneo nyeti. Bila shaka unapata kinyaa kuendelea naye lakini hapo siyo mwisho. Kuna kitu cha kufanya zaidi.
Itaendelea wiki ijayo...KHADIL KANTANGAYO

No comments:

Post a Comment