Saturday, January 1, 2011

KONA ZA WCHUMBA

2011 uyamiliki mapenzi, yakikumiliki utalia wiki 52


Tumshukuru Mungu kwa kutufikisha leo Mwaka Mpya. Wewe ni miongoni mwa wateule  waliouona mwaka 2011. Kwa kutambua hilo, nimeleta mada hii ili ikuwezeshe kumaliza salama siku 365, wiki 52 au miezi ya 12.

Kinyume chake ni kilio cha mwaka mzima. Mada hii itakuwa na lengo moja tu la kuwaponya wale wote wanaoishi kwenye mapenzi yasiyo na amani. Yale yanayoashiria kifo cha mapema na kuwafanya wabadili uelekeo.

Wanaweza kuanza kuheshimu kile kilichowaunganisha. Yaani kuufanya ‘uspesho’ wao uwe na maana. Ikiwa hivyo, basi watakuwa wanaondokana na jinamizi la kifo cha haraka. Hapa si utani, inahitaji utulivu kujua.

Msongo wa mawazo kila siku au mara kwa mara, husababisha mwili kushindwa kufanya kazi sawasawa. Athari kubwa huelekea kwenye moyo ambao ndiyo injini ya mwili wa binadamu.

Mapenzi ndiyo kitu namba moja kinachoweza kumfanya mtu awe na msongo mkubwa wa mawazo. Pesa au njia za pesa, ni kichocheo namba mbili lakini kina unafuu wake pale unapopata faraja kutoka kwa mwenzio.

Katika mapenzi, hakuna kinachoweza kukupa ahueni zaidi ya kuelewana na yule unayempenda hata kama amekuudhi, vinginevyo utakosa utulivu wako. Mapenzi yanaua lakini sizungumzii kunywa sumu.

Nazungumzia athari inayojengeka katika moyo baada ya kutokuwa kwenye maelewano chanya na mwenzi wako. Mwili unakosa upumuaji mzuri, hivyo kutema sumu ndani kwa ndani. Matokeo yake unajiona mgonjwa kumbe mapenzi.

NALIGUSA KUNDI HILI
Mtu hana maelewano na mwenzi wake, moyo unamlazimisha atafute suluhu lakini anakuwa mbishi. Anataka kujionesha kwamba yeye yupo salama na hatishiki kwa lolote.

Saikolojia inakutaka ujitunze usiumizwe. Yaani uwe na tahadhari kutafuta suluhu pale isipostahili lakini kama ishu ni ndogo, iweje isiwekwe mezani na kutafuta ufumbuzi?

Mara nyingi mtu huyu huumia sana baadaye hasa baada ya kugundua ukweli kuwa yule aliyekuwa anamfanyia ‘ushenzi’ ameshaondoka na pengine hatarudi tena kwake. Amechezea mawe, kapoteza almasi lakini majuto mjukuu!

HILI NALO LIMO
Ipo jamii ya watu ambao hutaka jamii iwaone wao ni ngangari katika mapenzi. Yaani hawawezi kuumia hata wafanywe nini. Wanajidanganya kwa ‘ubishoo’ wao. Kuna kitu utajifunza leo.

Ukweli ni kuwa hakuna mtu ambaye anaweza kujitenga na maumivu ya moyo pale anapoumizwa na mtu anayempenda. Anaweza kutabasamu akiwa na wewe lakini peke yake ni kilio cha ndani kwa ndani.

Yaani hayupo kwenye hali nzuri na mwenzi wake lakini eti anadhani akisema atachekwa. Ameshajiaminisha yeye ni ngangari lakini ikae kichwani kuwa mtu wa aina hii ni rahisi kufa.

Si kwa kujinyonga isipokuwa anaweza kuangamia taratibu. Hapa nataka nikupe pointi bora ya maisha kuwa; Fanya kila uwezalo kuhakikisha moyo wako unakuwa salama. Usiupe mzigo usio wa lazima.
Maumivu ya mara kwa mara ya kimapenzi ni mzigo mkubwa mno ambao huutwisha moyo wako. Masikini ya Mungu, wenyewe huwa hausemi kwa kutoa sauti ila unapoelemewa maumivu hukurudia mwenyewe.

USILISAHAU NA HILI
Wapo ambao huumizwa wao lakini kutwa kiguu na njia kutafuta suluhu. Haikatazwi kwa maana anatafuta amani ya moyo wake lakini muhimu ni je, huyo anayehangaikiwa yuko vipi?

Ni kujipa mzigo mzito kichwani kubembeleza penzi la mtu ambaye hana hisia na wewe hata kidogo. Bora uumie leo, tafuta faraja kwa watu wako wa karibu, omba kwa Mungu akuvushe salama katika kipindi kigumu.

Anakutenda leo, wewe ndiye unayepigana kutafuta amani irejee na upendo uendelee. Binadamu alivyo na hulka ya ajabu, ukifanya hivyo hawezi kukuona ni mtu bora, isipokuwa ataamini amekupata na huna ujanja, hivyo atarudia yale yale.

No comments:

Post a Comment