Lugha ni mfumo maalumu wa sauti nasibu za kusemwa unaotumika na jamii ya utamaduni fulani kwa ajili ya mawasiliano au kupashana habari. Lugha zote duniani zina tabia zinazofanana ingawa sababu hiyo haifanyi lugha zote kufanana japokuwa kuna zinazokaribiana. Lugha huathiriwa na lugha nyingine, lugha huweza kuongeza msamiati na mara nyingine huweza kufifisha msamiati na ukatoweka katika matumizi, hakuna lugha bora kuliko nyingine, kila lugha ni bora kwa kuwa inakidhi haja ya mawasiliano.
Sanaa ni ufundi wa kuwasilisha hisia na mawazo ya binadamu kwa mdomo, maandishi, michoro na uchongaji. Sanaa ya maandishi imegawanyika katika tanzu kuu tatu ambazo ni tamthiliya, riwaya na ushairi na tanzu hizo zina vipengele vidogovidogo. Sanaa ya uchoraji hujumuisha michoro ya mapangoni, michoro ya vikatuni na michoro mingine mingi, lengo lake likiwa kufikisha ujumbe kwa jamii. Sanaa ya uchongaji ni sanaa ambayo watu wachache kwenye jamii ndio wanaojishughulisha nayo kwani watu wenye ujuzi wa kuchonga ni wachache ambao hutoa mawazo yao kupitia vinyago wanavyovichonga. Sanaa za jukwaani ni sanaa ambazo hujumuisha nyimbo za miziki, maigizo na ngoma za kienyeji. Katika makala haya nitajikita zaidi kueleza uhusiano uliopo kati ya lugha na sanaa za jukwaani na kueleza zaidi kwenye umuhimu wa vionjo vya lugha katika sanaa.
UHUSIANO WA LUGHA NA SANAA
Lugha na sanaa ni vipengele muhimu vya utamaduni wa jamii yoyote, jamii huweza kujitambulisha popote pale kwa vipengele hivi kwani mtu anaweza kutambulika popote pale kwa kuongea lugha yake au akatambulika kwa sanaa yake kama vile ngoma, nyimbo n.k. Unapoongelea Sanaa iwe ya jukwaani au sanaa nyingine huwezi kukwepa lugha ambayo ndiyo mhimili mkuu wa sanaa yoyote ile. Sanaa hususani za majukwaani haziwezi kuvutia, kufikisha ujumbe, kuburudisha au kuonya kama matumizi ya nyenzo kuu (Lugha) haikutumika vizuri. Ili Sanaa iweze kukidhi haja ya hadhira lazima wawasilishaji wawe mahiri katika matumizi ya lugha na katika muktadha huu ni Lugha ya Kiswahili. Umahiri wa Lugha unaozungumziwa ni matumizi ya lugha fasaha ambayo inajumuisha sarufi, muundo na vionjo muhimu katika lugha kama vile, tamathali za semi, nahau, methali na misemo ambavyo vina uwezo mkubwa wa kusisitiza, kushawishi, kueleza kwa usahihi kile kilichokusudiwa pasipo kuwa na mlolongo wa maneno mengi.
VIONJO VYA LUGHA NA UMUHIMU WAKE
Katika lugha yoyote duniani vionjo vya lugha havikwepeki kwa kuwa ndivyo vinavyodhihirisha utajiri na msamiati wa kutosha katika lugha hiyo. Baadhi ya vionjo hivyo ni: tamathali za semi, nahau, methali na misemo.
Tamathili za semi
Tashihisi usemi wenye kukipa uhai kitu kisicho na hai (ukuta ule ukasogea
Kwa nguvu. Jiwe lile likasema)
Takiriri kurudiarudia, mkarara (sogea, sogea, sogea)
Tabaini usemi wenye dhana ya ukinzani lakini maana ya msingi haitenguki. Mfano yeye anatuona lakini sisi hatumwoni
Balagha usemi wenye kukuza jambo kuliko uhalisia. Kwa mfano: Kijana ana sikio kama la tembo, Ana kifua kama kabati
Tasifida usemi wenye kuvisha nguo maneno makali yatumikayo kwa lengo la kulinda maadili ya jamii. Kwa mfano anakwenda haja kubwa badala ya anakunya.
Nahau, misemo na methali
Nahau: Haya ni mafungu ya maneno yenye maana maalumu ambayo haitokani na maneno ya kawaida yaliyopo kwenye maneno hayo. Nahau za lugha yoyote hutumiwa zaidi na jamii yenye asili ya lugha hiyo. Kwa mfano Amezunguka mbuyu - amekula rushwa. Ana mkono wa birika –mtu mchoyo. Amekula chumvi nyingi- ameishi miaka mingi n.k.
Methali: Usemi wa kisanii wa kimapokea unaofikiriwa na jamii kuwa kweli na unaotumiwa kufumbia au kutolea mifano na huwa unabeba maana pana kuliko maneno yenyewe yanayotumiwa. Kwa mfano:- Hasira ya mkizi furaha ya mvuvi. Mcheza kwao hutunzwa. Mgaagaa na upwa hali wali mkavu.
Misemo: Ni mafungu ya maneno yanayotumiwa na jamii ya watu wa lugha hiyo kwa namna maalumu ili kutoa mafunzo, maadili na kuihadharisha jamii. Misemo ni maneno ambayo jamii huyatumia kutokana na uzoefu katika maisha. Kwa mfano: Mpaji ni mungu, aliye juu mngoje chini, Lila na fila havitengamani. Hata hivyo kutokana na maendeleo ya binadamu na utandawazi kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa misemo mingine imepitwa na wakati.
Vionjo vya lugha vilivyoainishwa hapo juu ni baadhi tu ya vichache kati ya vingi ambavyo huweza kuipamba, kuisherehesha na kuifanya lugha ifikishe ujumbe wake kwa usahihi. Sababu ya kutumia vionjo hivyo ambavyo ni chachandu katika sanaa ni kusisitiza na kutafuta mbinu za kufikisha ujumbe uliokusudiwa. Kuna msanii mmoja ambaye amepata umaarufu mkubwa kutokana na mtindo wa sanaa yake ya kuimba nyimbo ambazo karibu robo tatu ya wimbo una misemo ya Kiswahili ya wahenga na mingine akiibuni yeye mwenyewe.
LUGHA SANIFU KATIKA SANAA
Ni ukweli usiopingika kwamba ili ujumbe ufike kwa aliyekusudiwa ni muhimu nyenzo ya kuufikisha isiwe na utata. Kumekuwa na matumizi ya lugha ambayo si sanifu na fasaha na matokeo yake kwa mgeni ambaye amejifunza lugha sanifu si rahisi kupata ujumbe uliokusudiwa na msanii. Msanii ni kioo cha jamii na wasanii wana ushawishi mkubwa wa kuikengeusha jamii wanapokusudia. Mara nyingine wanafanya kazi kwa kubahatisha kwani wataalamu wa kurekebisha lugha ambayo ni nyenzo yao kuu katika kazi zao wapo na wanapatikana muda wote lakini hawawatumii. Wasanii wengi ambao nyimbo zao zimekuwa, zikitamba ni wale ambao wameitumia lugha ya Kiswhaili vizuri ikiwemo matumizi ya vipengele ambavyo tumevitaja hapo juu.
UKENGEUSHI WA MAANA ZA MSAMIATI
Nimeanza makala kwa kusema lugha ni Sauti za nasibu na unasibu huu ulitaja kila uwakilishi wa vitu vilivyopo kwenye jamii hiyo. Matusi yote yana uwakilishi wake ambao ukiutaja hadharani lazima ukapimwe akili. Lakini maneno haya yanayonyang’anywa eti kwa kuwa yanafananishwa na yale ambayo hatuyataji hadharani si sahihi.
UKOSEFU WA UBUNIFU WA KUTOSHA WA WASANII WA SANAA ZA JUKWAANI
Zamani wasanii walikuwa na sanaa ambazo zilikuwa zinafuata kanuni na utaratibu wa sanaa. Wasanii wa zamani walikuwa wakiimba nyimbo za malumbano na za kusemana lakini ilikuwa si rahisi kugundua hasa kama una umri mdogo na hujawa mahiri katika lugha. Je hali iko hivi leo? tutajadili kwa pamoja. Angalia kipande cha shairi la Muyaka Bin Haji enzi hizo akiwasema wakoloni juu ya ubaya wao.
Lahaja: Mbwene shumndwa na Mbuzi wachandamana pamoya
Na mwana kuku na Kozi wachilea wao wana
Na mtu msi maozi, akionya watu ndia
Hayano si kuambiwa niwene kwa mato yangu
Sanifu: Nimemuona Fisi na Mbuzi wakiandamana pamoja
Na mwana Kuku na mwewe wakilea watoto wao
Na mtu asiyeona akionyesha watu njia
Haya sikuambiwa nimeona kwa macho yangu
Shairi hili la Muyaka lilikuwa linawapa urazini Waafrika juu ya namna wanavyoishi na watu ambao walikuwa ni maadui wao. Ujumbe huu alikuwa anawapa Waafrika wenzake bila kugunduliwa na wazungu wachache ambao kwa kuwa Kiswahili si lugha yao ya kwanza ilikuwa vigumu kukipata kilichokuwa kinasisitizwa.
Ni wasanii wachache ambao wamekuwa wabunifu au kusoma kazi za wahenga ambao walikuwa mahiri wa lugha. Tunafahamu kuwa Fasihi inaishi na haifi ndio maana hata leo unaweza kusema shairi la Muyaka bado linasadifu “Bado Fisi na Mbuzi wanaandamana pamoja, Mwana kuku na mwewe wanalea wana wao na Wanaoonyeshwa njia na vipofu bado tunaishi nao ingawa ni wachache,
HITIMISHO
Katika fasihi tunaelezwa kuwa unapotaka kuichambua kazi ya fasihi lazima kuwe na fani na maudhui na tunasisitizwa kuwa fani ambayo huibeba lugha ikisukwa vizuri ujumbe ndivyo utakavyoifikia jamii kama ilivyokusudiwa na msanii. Hivyo ni vyema wasanii wetu wakatambua kuwa lugha ndiyo inayofanya kazi ya sanaa ipendeze. Wasanii wote wanaotamba na kazi zao nzuri ni wale wanaojua kucheza na lugha na si vinginevyo. Kumbuka unavyocheza na lugha ndivyo unavyofikisha maudhui mengi kwa wakati mmoja.
BY KHADIL